desktop logo

EXPLORE

DATA

twitterfacebook
mobile logo
news
Je, Kuna Matumaini ya Kuafikia Malengo ya Afya kwa Wote?
June 2022
PesaYetu
article

Share

By Peter Mutua 

Katiba ya Kenya inaelezea kuwa ni haki ya kila mkenya kupata huduma za afya za kiwango cha hali ya juu iwezekanavyo. Ni kwa sababu hii rais Uhuru Kenyatta akitoa ajenda nne kuu za serikali yake, alisisitiza umuhimu wa utoaji afya kwa wote yaani UHC ifikiapo mwaka wa 2022. 

Malengo kuu ya mradi huu ni kuhakikisha kuwa kila mkenya anapata huduma za afya hitajika pasi na kutatizika kifedha. Hatua kadhaa zimepigwa katika kutekeleza mradi huu wa UHC. 

Miswada mbalimbali imewasilishwa bungeni na kupitishwa ambayo inakusudia kupunguza changamoto za kifedha ambazo huambatana na utoaji huduma kwa umma. Mpango huu umeimarisha sekta ya afya haswa kwa wachochole nchini ambao aghalabu hufanya kazi za kijungu jiko.

Hata hivyo, changamoto zipo kwa wingi na licha ya miswada kupitishwa bungeni, donda sugu limebakia changamoto za kimsingi kama vile ukosefu wa dawa hospitalini na migomo ya mara kwa mara ya wauguzi na madaktari.

Wakati wa uzinduzi wa kaunti nne za kwanza ambapo mradi wa UHC ungeng’oa nanga, kaunti ya Isiolo ilikuwa mstari wa mbele kukumbatia mradi huo. Kauti ya Isiolo ilitengewa asilimia 28 za pesa hizo ikiwa ni 285 milioni, hata hivo mradi huo uliwahakikishia wakenya kuwa kila mwananchi mwenye kadi ya UHC anapata matibabu pasi na kutatizika kifedha. Kadi hizo zitatumika katika hospitali za umma kama bima ya kulipia matibabu ila aliyejiandikisha atahitajika kulipa ada kila mwaka. Ada yenyewe ni nafuu kwa kila mkenya.

Hata hivyo, takriban miaka miwili baada ya kuzinduliwa kwa mradi huo, matatizo yameukumba si haba. Kaunti zilizokuwa zimeuanzisha mradi huo zikiusitisha kwa tuhuma za kukosa fedha kutoka kwa serikali kuu. 

Isitoshe, wanaoishi mashinani katika kaunti ya Isiolo haswa maeneo ya Oldonyiro na Gotu wanaelezea kuwa licha ya serikali kupunguza ada ya kupata matibabu hospitalini, changamoto za kimsingi kama ukosefu wa barabara zinazidi kuwatatiza.

Kwa mfano kutoka Oldonyiro kuja katika hospitali ya rufaa ya Isiolo ni takriban kilomita 160, umbali ambao unalichukua gari Zaidi ya masaa tatu kusafiri. Hii ni licha ya changamoto za barabara mbovu na ukosefu wa usalama kutokana na vita vya kijamii vya mara kwa mara.

Aidha, ukosefu wa usafiri wa umma katika baadhi ya maeneo katika kaunti ya Isiolo ni donda sugu linalotishia maisha ya wakaazi wanaohitaji msaada wa afya. Kwa wale walio na magari binafsi, wanatoza nauli ya juu zaidi kwa kuwa barabara ni mbovu. Matatizo yanajiri lich ya serikali ya kaunti kukadiria kutenga zaidi ya shilingi bilioni tatu katika kipindi cha miaka tano kutoka 2018 hadi 2022. 

Vile vile, inasikitisha kuwa hata baada ya serikali kuondoa ada za msingi katika hospitali za umma, baadhi ya wahudumu wa afya wangali wanatoza ada hizi. Hata hivyo, wahudumu wa afya pia wameinyooshea serikali kidole cha lawama. Baadhi ya hospitali ambazo zinakubali kadi ya UHC zinaelezea kuwa licha yao kutaka kuwasaidia wakaazi, ucheleweshaji wa fedha kutoka kwa bima hiyo kunatatiza utoaji huduma. Vile vile hospitali nyingi za umma hazina vifaa muhimu na  hata dawa hukosekana kwa muda mrefu na kuwafanya wenyewe kutamauka.

Ni wajibu wa serikali kuhakikisha kuwa miswada inayopitishwa inatekelezwa vilivyo. Pia ni wajibu wa viongozi waliochaguliwa kuhakikisha kuwa miradi ya serikali inazingatia hatua hitajika kulingana na umuhimu wake. Si vyema kupunguza ada ya afya iwapo vituo vya afya havipo.Ni muhimu kushughulikia mambo muhimu na ya msingi kwanza kabla ya kuanza miradi ambayo itagharimu mabilioni ya pesa na mwishowe kutomnufaidi mkaazi.

Image: Wagonjwa hospitalini Isiolo. Source: Devex

Makala haya yameandaliwa na Shahidi FM kwa kushirikiana na Code for Africa, Kenya Community Media Network (KCOMNET)  na Baraza la vyombo vya habari katoliki (CAMECO) kupitia msaada wa Ujerumani kama sehemu ya mradi wa kaunti yetu , jukumu letu.

Related Stories
Usambazaji wa Umeme Jijini Nairobi
By Sharon Gitonga Mkakati wa kuunganisha umeme ni swala ambalo lilipewa kipaumbele pindi tu serikali ya Jubilee ilipojinyakulia uongozi mnamo mwaka wa 2013. Mradi huu umeshuhudiwa kupanuka kwa kasi katika mji wa Nairobi. Sababu kuu  ni kumwezesha mwanachi wa kawaida kujimudu kimaisha. Kulingana na ripoti la CDIP,  jijini Nairobi, takribani asilimia tisini na tano ya […]
logo
This site is a project of Code for Africa, the continent’s largest network of civic technology and data journalism labs. All content is released under a Creative Commons attribution Licence 4.0. Reuse it to help empower your own community.

2022 PesaYetu

Resources
  • About
  • Privacy Policy
  • Terms of Service
Stay in touch with us
instagramfacebooktwitterlinkedin